Monday , 8th Feb , 2016

Mamlaka ya chakula na dawa TFDA kanda ya kati imekamata shehena ya bidhaa zilizokuwa zimehifadhiwa kinyume na taratibu ikiwemo chooni na zilizokwisha muda wa matumizi katika kata ya kihonda manispaa ya Morogoro hali inayohatarisha afya za watumiaji.

Hali hiyo imebainika wakati wa mwendelezo wa zoezi la ukaguzi linalofanywa na TFDA mkoani Morogoro ambapo ilifanikiwa kuingia kwa mfanyabiashara aliyetambulika kwa jina moja la Shabani,anayedaiwa awali kukamatwa na maofisa wa mamlaka hiyo na kutozwa faini ya shilingi laki sita baada ya kukutwa amehifadhi vinywaji maeneo ya sambamba na bidhaa zilizo kwishwa muda wake wa matumizi.

Mfanyabiashara huyo pamoja na kuahidi kuteketeza, amegunduliwa kushindwa kufanya hivyo.

Baada ya maofisa wa TFDA kutilia mashaka,wamerudia kufanya ukaguzi mwingine wa kushtukiza kwa mfanyabiashara huyo na kukuta hali ikiendelea kama awali.

Zoezi hilo awali liliingia ugumu baada ya mfanyabiashara huyo kugoma kufungua geti kwa maelezo kuwa hakuwa mhusika, huku EATV kupitia upenyo ikibaini, mtuhumiwa kuhamisha kinyemela bidhaa hizo ndani jambo lililowalazimu maofisa hao kuingia kwa nguvu ili kudhibiti hali hiyo.

Ukaguzi uliofanywa umegundua udanganyifu uliokuwa ukiendelea kufanywa na mfanyabiashara huyo kwa kushindwa kuteketeza bidhaa alizokuwa ameagizwa, badala yake aliamua kuuza baadhi yake.

Pamoja na maofisa hao kuahidi kujipanga kwa mbinu zaidi kukabiliana na wafanyabiashara wakaidi, walimuamuru kufungwa kwa duka hilo na kusitishwa shughuli zote za biashara hadi pale kesi inayotarajiwa kufikishwa mahakamani ikiwemo kwa kukaidi amri ya mamlaka hiyo itakapotolewa maamuzi,na maofisa hao wameteketeza baadhi ya bidhaa zilizokamatwa zikiwa zimekwisha muda wa matumizi..