Tuesday , 15th Jul , 2014

Serikali ya Tanzania leo imetiliana saini makubaliano ya mkataba wa kupata fedha zaidi ya shilingi bilioni 108 za Tanzania kutoka kwa wadau wa maendeleo, fedha ambazo zitatumika katika kuboresha sekta ya afya nchini.

Katibu mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi Dkt Servacius Likwelile (kulia) akisaini moja ya makubaliano na balozi wa Jumuiya ya Ulaya nchini Tanzania Filberto Sebregondi.

Akizungumza mara baada ya kutiliana saini makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa wizara ya fedha na uchumi Dk. Servacius Likwelile amesema fedha hizo zitatumika katika kununulia vifaa vitakavyotumika katika hospital za serikali pamoja na kupanua miundo mbinu ya hospital hizo.

Kwa upande wake Katibu mkuu wa wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini Tanzania Charles Palanjo amesema lengo ni kuhakikisha hospitali pamoja na vituo vya afya vya serikali vikiwemo vya vijijini na mijini vinakidhi mahitaji yakiwemo ya Dawa na huduma nyinginezo.

Palanjo amesema asilimia 74 ya fedha hizo zitakwenda katika halmashauri za wilaya kwa lengo la kununua madawa pamoja na vifaa tiba huku nyingine zikitumika kusaidia kujenga uwezo kwa watumishi katika sekta ya afya.