Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema Taifa lina uhaba mkubwa wa damu salama lakini wananchi hawana mwamko wa kuchangia damu kwa kuwa hata kama wakichangia wanapokuwa na wagonjwa hutakiwa kununua damu hiyo.
Akizungumza leo kwenye maadhimisho ya kuchangia damu salama yaliyofanyika kitaifa kwenye uwanja wa Nyerere square Mwalimu alisema kuwa tabia ya waganga Wakuu wa Hospitali za Wilaya na Mikoa kuwauzia damu wagonjwa ndio chanzo kikubwa kunachopelekea wananchi kutokuwa na moyo wa kuchangia damu.
Ametoa wito kwa waganga wote waliopo kwenye vituo vya afya vya serikali na hospitali zote za mikoa nchini kuweka mabango yanayoelezea kuwa damu haiuzwi bali inatolewa bure.
“Wananchi wengi wako tayari kuchangia damu lakini wanakwamishwa na kuchangia damu bure kesho anamgonjwa wake anaambiwa alipe na hili ndio linawakwaza wananchi wengi lazima waganga na wakuu wa mikoa wahakikishe wanatoa urasimu katika suala hilo”alisema Waziri Ummy
Kwa upande wake meneja wa mpango wa damu salama nchini, Dk, Abdu Juma amesema kuwa Taifa bado lina changamoto kubwa ya uhaba wa damu salama hali inayohatarisha uhai wa watoto wadogo, akina mama wajawazito na majeruhi wa ajali mbalimbali.
“Endapo kama halmashauri zote zitaweza kukusanya damu tulivyopanga tuatweza kukusanya chupa hadi elfu ishirini, lakini pia kwa mkoa wa Dodoma tumeweka malengo ya kukusanya chupa 600 kwa siku tatu hadi hivi sasa tumeweza kukusanya chupa 452 hivyo tunaamini tutafikia lengo na kuvuka lengo” alisema Dkt Juma.