Waziri wa maliasili na utalii wa Tanzania, mheshimiwa Lazaro Nyalandu.
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na serikali ya Marekani wameandaa mkutano unaolenga kujadili uhifadhi wa wanyamapori katika hifadhi zote nchini hususani wakianza na hifadhi ya Selous.
Hayo yameelezwa leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Mali asili na Utalii, Mhe Lazaro nyalandu wakati akipokea helikopta iliyotolewa na tajiri wa Marekani Buffet Haward kwa ajili ya kupambana na tatizo la ujangili wa wanyamapori.
Waziri Nyalandu amesema mkutano huo utafanyika Juni 27 mwaka huu, jijini Dar es Salaam ili kuangalia namna ya kukabiliana na uhalifu wa wanyamapori.
Taarifa za kufanyika kwa mkutano huo zimekuja siku moja baada ya ripoti ya taasisi ya kimataifa inayopambana na ujangili pamoja na biashara haramu ya wanyama walio katika hatari ya kutoweka ya CITES, kuelezea kuridhishwa na juhudi zinazofanywa na serikali za nchi za Afrika Mashariki katika kupambana na ujangili hususani wa wanyama jamii ya tembo.