Thursday , 19th Jun , 2014

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na vyombo vya usalama vya kimataifa imeahidi kuhakikisha usalama wa raia na mali zao ikiwa ni pamoja na kutambua vyanzo vya matukio ya kihalifu na mipango ya kihalifu kabla haijatekelezwa.

Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda akijibu swali la Mhe. Betty Machangu Bungeni Mjini Dodoma hii leo aliyetaka kufahamu hatua zinazochukuliwa na serikali kudhibiti makundi ya kihalifu yaliyotapakaa nchi nzima kama kundi la Panya Road.

Mhe. Pinda amesema kuwa hali ya usalama kwa sasa ni shwari kwani serikali imechukua hatua madhubuti kuhakikisha inadhibiti makundi ya aina hiyo, hata hivyo amewataka vijana kujiepusha na vitendo ambavyo vitawafanya wajikute mikononi mwa vyombo vya dola.

Aidha jijini Dar es Salaam, wazara ya elimu na mafunzo nchini Tanzania imesema imeanza kushughulikia ukosefu wa vifaa vya kufundishia pamoja na kuboresha mazingira ya kufundishia walimu katika shule za msingi na sekondari nchini ili kufanikisha mpango wa matokeo makubwa sasa kwa kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.

Afisa Elimu Mkuu wa kitengo cha matokeo makubwa sasa kutoka wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bi. Hilder Mkandawile amesema kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa elimu ya msingi nchini kimeongezeka kutoka asilimia 35 na kufikia asilimia 58 mwaka huu huku kwa sekondari kikiwa kimeonezeka kutoka asilimia 43 hadi asilimia 51 kutokana na mpango huo .

Bi. Mkandawile amesema serikali imeendelea kujenga uwezo wa mwalimu katika kubaini wanafunzi mbalimbali wenye uwezo hafifu ili kumpa mwalimu fursa ya kuwaangalia zaidi pamoja na kutoa kipaumbele kwa walimu walio katika mazingira magumu.