Tuesday , 9th Feb , 2016

Serikali imesema itaendelea kudumisha na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi rafiki na wadau wa maendeleo ili kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na kutimiza malengo ya mpango wa maendeleo endelevu

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustino Maiga akizungumza, Dar es Salaam

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dkt. Augustine Mahiga kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, wakati wa hafla ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2016 iliyoshirikisha mabalozi mbalimbali wanazoziwakilisha nchi zao hapa nchini iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam.

Balozi Mahiga amesema ifikapo mwaka 2030 Tanzania itakuwa imepunguza kiwango cha umasikini na kuboresha maisha ya watu nchini.

“Hivi sasa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania Bara umekwisha. Ni wakati wa kufanya kazi na kauli mbiu yangu ni “Hapa Kazi Tu”. Serikali mpya ya awamu ya tano imekuja na mkakati wa kuboresha na kuimrisha utendaji kazi katika utumishi wa umma ili kusisitiza nidhamu na utendaji kazi, kuheshimu haki za binadamu, utawala bora na kuhakikisha wananchi wote wa Tanzania wanapata maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii,” alisema Balozi Mahiga.

Balozi Mahiga aliongeza kwamba Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ameiacha nchi ikiwa imara na marafiki wengi, pia uchumi wake umekuwa katika kiwango cha asilimia saba (7) kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Alisema mafanikio hayo yametokana na juhudi za ushirikiano na misaada yao, hivyo aliwashukuru kwa michango yao waliyoifanya hapa nchini.

“Ninawaomba muendelee kutusaidia kwa kuwa hivi sasa tuna mipango ya maendeleo ambayo ina lenga kuboresha maisha ya Watanzania wote hususan wale wanaoishi katika kiwango cha chini cha umasikini,” alisema Balozi Mahiga.

Alizitaja changamoto kubwa zilizopo katika kutimiza malengo hayo ni kuwepo kwa hali ya umasikini nchini, ukosefu wa ajira na rushwa.

Hivyo Serikali inafanya kila jitihada za kukabiliana na changamoto hizo kwa kuwa bila ya kufanya hivyo itakuwa ni vigumu kutimiza malengo ya nchi ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Balozi Mahiga alisema kwamba ili kutimiza malengo hayo, serikali hivi sasa inaendelea kudhibiti matumizi ya fedha za serikali, kujenga nidhamu, uwazi na uwajibikaji katika matumizi hayo ndani ya serikali na hata kwa sekta binafsi na kuimarisha maeneo ya ukusanyaji wa mapato.

Aidha, serikali imesema kwamba itaendelea kuendeleza ushirikiano huo, ili kuweza kupambana na vitendo vya rushwa, biashara haramu ya binadamu, ugaidi na matumizi ya silaha.

“Tunawaomba mtusaidie husasan kwenye eneo la upatikanaji wa taarifa, kujenga uwezo na masuala ya kiufundi katika kukabiliana na vitendo hivi,” alisema.

Akizungumzia kuhusu suala la uchaguzi wa Zanzibar, Balozi Mahiga alisema Zanzibar inajitegemea katika masuala ya kisiasa na kiutamaduni licha ya kuwa ni sehemu ya Muungano wa Tanzania.

Balozi Mahiga alifafanua kuwa Zanzibar ina Katiba yake, Serikali na Tume Huru ya Uchaguzi .Hivyo kutokana na matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015 ulifutwa kwa sababu mbalimbali kama ilivyoelezwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar(ZEC).

Aliongeza kwamba mazungumzo ya kufikia muafaka wa suala hilo, yanaendelea ma uchaguzi mwingine utafanyika Machi 20, mwaka huu. Hivyo mazungumzo hayo bado yanaendelea ili kuufanya uchaguzi huo uwe huru, haki na uwazi ili kukidhi viwango vya kimataifa vya demokrasia.