Wednesday , 23rd Mar , 2016

Wazee wa Mkoa wa Tanga wamemtaka Mkuu mpya wa Mkoa huo Martine Shigela, kuharakisha kumaliza mvutano wa halmashauri ya Jiji la Tanga, ili kuharakisha maendeleo ya Jiji hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella

Wazee hao wametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha pamoja na Mkuu wa Mkoa huyo kilichowakutanisha ili kujadili changamoto zinazoukabili Mkoa huo ikiwemo kutatua kero zinazowakabili wakazi wa Mkoa huo.

Wazee hao wamesema madiwani hao kuendelea na mvutano huo ni kuwanyima haki wananchi waliowachagua kutokana na hadi leo kushindwa kujadili bajeti ya mkoa ambapo wamemshauri kama ikishindikana ni bora halmashauri hiyo ikavunjwa.

Kwa upande wake Meya wa Jiji la Tanga ambae anapingwa na baadhi ya madiwani wa Jiji hilo la Tanga Mustapha Selebosi amewataka wazee hao kutokata tamaa ya kusuluhisha mzozo na badala yake waendelee kutengeneza historia ya jiji hilo badala ya kuwa na mawazo ya kulifuta jiji hilo.

Kwa upande wake Mkuu huyo wa Mkoa wa Tanga Martine Shigela amesema kuwa anachojali yeye ni maendeleo ya Mkoa huo na sio kutaka kujua Meya wa jiji ni nani au wa chama kipi hivyo wataendelea kujadili bajeti ya mkoa huo bila baadhi ya madiwani.