Monday , 15th Feb , 2016

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema hana taarifa zilizomfikia kama kiongozi wa juu wa Serikali ya Mapinduzi, kuhusiana na kuwapo kwa kikundi cha vijana wanaopiga watu katika baadhi ya maeneo, maarufu mazombi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi

Hata hivyo balozi Seif ameviagiza vyombo vya ulinzi kufanya uchunguzi dhidi ya shutuma hizo na pale itakapobainika kuwepo kwa ukweli wa shutuma hizo vifanye juhudi ya kuwakamata wahusika hao na kuwafikisha mbele ya dola ili sheria ichukue mkondo wake.

Aliwaasa na kuwaomba wananchi wa maeneo mbalimbali kisiwani Pemba kuendelea kuishi kwa amani na upendo na kushirikiana katika mambo yao bila ya kuendekeza zaidi itikadi zao za kisiasa ambazo tayari zimeshaonesha muelekeo mbaya.

Balozi Seif alieleza kwamba matokeo ya sasa yaliyojichomoza katika hujuma za moto sambamba na baadhi ya watu kuanza kuashiria vitisho dhidi ya wananchi wenzao walioamua kushiriki uchaguzi wa marejeo kwa kuwatilia X nyumba zao yanaonesha safari ya hatari katika maisha miongoni mwa jamii.