Friday , 8th Jun , 2018

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Lameck Nchemba amesema Waraka wa barua unaodaiwa kuandikwa na serikali dhidi ya Makanisa unaosambaa mitandaoni si wa kweli na kwamba huo ni uhalifu uliofanywa na watu wasioitakia nchi mema.

Waziri Nchemba ametoa ukanusho huo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi  ya Makao Makuu ya Mambo ya Ndani jijini Dar es salaam.

Amesema serikali haipingani na dhehebu lolote nchi na kwamba pale ambapo kunakuwa na  uhitaji wa kufanyia kazi jambo kuhusu taasisi hizo zilizopo chini ya wizara hiyo taratibu huwa zinatumika kuzungumza na sio kama ilivyofanywa  kwenye taarifa hiyo inayosambaa.

Pamoja na hayo waziri huyo ameongeza "Serikali inalinda uhuru wa kuabudu na waumini hivyo taarifa hiyo inayosambaa ni batili na tayari uchunguzi umeanza kufanyika. Watu waache kuweka misimamo bila kuwa na uhakika wa taarifa kutoka serikalini ambao ndiyo wahusika wakutoa taarifa kisheria" .

Mbali na hato Waziri Nchemba ameonya wanasiasa wanaoingilia jambo hilo kisiasa kwa kusema kwamba kama umakini usipowekwa amani ya nchi itavurugika na ingawa bado wanaendelea na uchunguzi kuwabaini wahusika ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.