Tuesday , 27th Sep , 2016

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini imelazimika kutoa ufafanuzi wa hali ya upatikanaji wa dawa nchini baada ya kuripotiwa kuwepo kwa upungufu mkubwa wa dawa katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Dkt. Mpoki Ulisubisya

Akitolea ufafanuzi juu ya suala la upungufu wa dawa nchini Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema kuwa kuanzia mwaka wa fedha 2015/2016 MSD ilianza utaratibu wa kununua dawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ikiwa ni jitihada za kuhakikisha kuna upatikanaji endelevu wa mahitaji ya dawa kwa wananchi.

Amesema Serikali kupitia MSD tayari wamepokea makopo 10,000 ya vidonge vya dawa aina ya Paracetamol ambayo wamekwisha sambaza kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Aidha, amesema mkataba baina ya MSD na mtengenezaji wa ndani wa dawa hiyo wenye makopo mengine 138,000 ya vidonge vya Paracetamol yenye ujazo wa vidonge 1,000 umekamilika, ambapo dawa hizo zinategemewa kuanza kupokelewa kuanzia wiki ya kwanza ya mwezi wa Oktoba 2016.

Amesema dawa nyingine zilizokuwa zinahitajika zaidi ambazo ni Antibiotics na dawa za kupunguza maumivu (Ciprofloxacin, Ceftriaxone, Diclofenac, Co-trimoxazole , Amoxycline, Doxycycline na Metronidazole) zimewasili Makao Makuu ya MSD na tayari zimekwisha pelekwa kwenye kanda zote za MSD tayari kwa kusambazwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Amesema kwa sasa hali halisi ya upatikanaji wa dawa MSD ni sawa na 53% kwani kati ya dawa muhimu 135 zinazohitajika ghalani kuna aina 71 ya dawa hizo na nyinginezo ziko kwenye vituo vya kutolea huduma.

Kuhusu tatizo la chanjo, amesema kuwa upatikanaji wa chanjo nchini utaimarika zaidi kuanzia tarehe 2 Oktoba, 2016 baada ya kupokea shehena mpya na kuwaomba waganga wakuu wa wilaya na mikoa kuangalia mwenendo wa shehena zao na kutoa mgao mpya kwenye maeneo yenye upungufu pale kadhia hiyo itakapotokea.