Monday , 27th Jun , 2016

Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye amesema serikali imekubali kurusha matangazo ya bunge ya moja kwa moja kupitia redio nchini.

Mhe. Nnauye amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kituo cha matangazo ya redio ya kijamii inayolenga kuwafikia wananchi wa maeneo ya vijijini kwa ufadhili wa shirika la kimataifa la UNESCO. Nakusema kuwa baada ya wadau wa habari, waandishi wa habari na wabunge kukaa na kuangalia kwa kina suala hilo sasa redio zitarusha matangazo hayo.

Nape ameongeza kuwa yeye kama waziri wa habari anathamini sana uhuru wa kupata habari na demokrasia na kuwa uamuzi wa kusitisha urushwaji wa bunge live kwa njia ya televisheni uliamuliwa na bunge katika serikali iliyopita hivyo serikali ya sasa haiwezi kuwanyima wananchi haki yao ya msingi.

"Mimi ni muumini wa demokrasia, hatuwezi kuwanyima wananchi haki yao hivyo serikali ipotayari kukaa na wadau, waandishi wa habari pamoja na serikali na mazungumzo yanaendeleo. hivyo mapendekezo yetu nikuwa redio zitarusha matangazo ya moja kwa moja," alisema Nnauye.

Nape amesema, kwa awamu hii redio zitapokea matangazo kupitia studio ya habari ya bunge suala ambalo amesema litakuwa nafuu kwa redio hizo kwani hawata lazimika kutuma waandishi wa habari au kufunga mitambo yao Bungeni Dodoma kupata matangazo hayo.

Akiongelea mchango wa redio za kijamii, Mhe. Nnauye amesema serikali yake inadhamini na kutambua redio zote za kijamii kwani zimekuwa zikiisaidia serikali kuwafikia wananchi wapembezoni na kuwahabarisha juu ya masuala mbalimbali ya kiafya na kisera.

Aidha, Nnauye amewataka waandishi wa habari kuwa makini na kutanguliza maadili wa tasnia yao mbele kwani kila taarifa inayowafikia wananchi kinyume na ilivyo paswa inapotosha na kuiweka jamii katika hatari ya kupata taarifa zisizo sahihi.