Thursday , 7th May , 2015

Wakunga mkoani Njombe wamefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama wakati wa kujifungua mwaka jana kutoka 27 mwaka juzi na kufikia 21 ambapo zaidi ya wanawake 23,000 walifika kituoni kujifungua.

Mkuu wa wilaya ya Njombe Sarah Dumba akizungumza na wadau wa maendeleo (hawapo pichani)

Akizungumza mkoani Njombe, mratibu wa uzazi na mtoto mkoa Felisia Hyera, amesema kuwa kati ya wanawake 23,736 waliojifungua mwaka 2014 akina mama 21 walifariki kutokana na matatizo wakati wa kujifungua.

Hyera ameongeza kuwa kiwango cha wajawazito kujifungulia katika vituo vya afya kimeongezeka kwa asilimia 94 mwaka jana huku mwaka juzi ilikuwa ni asilimia 90.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Njombe Sarah Dumba amesema kuwa miaka ya nyuma kulikuwa na gumzo kwa akina mama wakienda hospitali hasa hospitali ya Kibena kuwa wakifika huko wanafariki.