Friday , 24th Apr , 2015

Serikali imekitaka kituo cha uongezaji thamani madini ya vito, kilichopo mkoani Arusha, kutoa mafunzo kwa vijana wa kike darasa la saba na kidato cha nne, bila masharti, ili waweze kupata ujuzi wa ukataji na ung'arishaji madini hayo.

Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene akiongea na Wanahabari.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, wakati akifungua kituo hicho, kilichoanza kutoa mafunzo mwaka jana Novemba na jana kufanikisha kuhitimu kwa wasichana 15, waliojifunza miezi sita, kukata na kung’arisha madini ya vito.

Amesema anaamini kundi kubwa la vijana wa madarasa hayo wakipatiwa kipaumbele kupewa mafunzo hayo, wataweza kujiajiri wenyewe na kujiinua kiuchumi, huku taifa likipata mapato kwa kuyaongezea madini hayo thamani.

Simbachawene amesema vijana wa darasa la saba na kidato cha nne ni wengi, na sekta hiyo inaweza kupunguza tatizo la ajira kwa asilimia 40, endapo mpango huo utakuwa endelevu kwa kundi hilo tu.

Amesema serikali imetumia zaidi ya Shilingi bilioni 3.4, kujenga kituo hicho na kununua vifaa vya ufundishaji, ili kuwainua vijana wa kike, ambao hawawezi kufanya kazi ngumu za uchimbaji madini.

Naye mwakilishi wa katibu mkuu wa wizara ya Nishati na Madini, Mrinia Mchovu, amesema kuwa kituo hicho kimeanzishwa ili kuongeza thamani ya madini nchini.

Pia serikali itaendelea kukiboresha kwa kutoa kozi za utengenezaji mapambo ya madini na uchongaji wa vinyago vya mawe ya madini, ili kuweza kuongeza kipato kwa mfanyabiashara na serikali.