Thursday , 26th Feb , 2015

Baadhi ya wananchi waliofika katika vituo mbalimbali vya uandikishaji katika daftari la wapiga Kura wameiomba serikali kuongeza siku za zoezi hilo kutokana na changamoto lukuki zinazokabili zoezi hilo.

Wakati zoezi la uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura kwa mfumo wa BVR likiingia katika siku ya Nne katika halmashauri ya Makambako mkoani Njombe baadhi ya wananchi waliofika katika vituo mbalimbali vya uandikishaji wameiomba serikali kuongeza siku za zoezi hilo kutokana na changamoto lukuki zinazokabili zoezi hilo.

EATV imetembelea baadhi ya vituo vya uandikishaji na kukuta misururu mirefu huku wananchi wakielezea jinsi hali ilivyo wengine wakidai kupanga foleni kuanzia siku ya kwanza zoezi hilo lilipoanza lakini hawajafanikiwa kuandikishwa hadi leo licha ya kupanga foleni kuanzia usiku wa manane kwa siku tatu mfululizo.

Baadhi ya akina mama wamesema kutokana na changamoto za mifumo kufanya kazi taratibu huku mwamko wa kujiandikisha ukiwa mkubwa kwa wananchi wanalazimika kuamka usiku wa manane kusimama kwenye misululu lakini licha ya hali hiyo kuhatarisha ndoa zao bado hawajui lini hasa watafanikiwa kujiandikisha na kupata vitambulisho hivyo vya kupigia kura.

Kwa upande wao mawakala wa vyama vya siasa wameshauri zoezi hilo liongezwe muda badala ya muda wa siku Saba uliopangwa kwani hakuna namna zoezi hilo linaweza kukamilika na kumaliza watu wote wanaojitokeza kutaka kuandikishwa kwani idadi ni kubwa mno kulinganisha na muda.

Katika siku ya uzinduzi wa zoezi hilo uliofanywa na waziri mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania mheshimiwa Mizengo Kayanza Pinda mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi Jaji mstaafu Damian Lubuva aliahidi kuwa hakuna mtu atakayeachwa bila kujiandikisha kwa sababu ya muda ikiwa atajitokeza kujiandikisha