Thursday , 6th Nov , 2014

Serikali imeomba fedha kutoka Wizara ya Fedha na Uchumi ili iweze kuharakisha kuwakopesha wanafunzi wa elimu ya juu zaidi ya 8,000 waliokosa mikopo.

Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda amesema serikali imeomba fedha kutoka Wizara ya Fedha na Uchumi ili iweze kuharakisha kuwakopesha wanafunzi wa elimu ya juu zaidi ya Elfu Nane waliokosa mikopo baada ya serikali kuongeza idadi ya wanafunzi wa masomo ya Sayansi.

Amesema hiyo ni kutokana na kuwepo kwa upungufu wa fedha katika bodi ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya juu nchini Tanzania na kusema serikali imepeleka maombi Wizara ya Fedha ili kuweza kutatua tatizo hilo linalowakabili wanafunzi hao.

Akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mhe. Kabwe Zitto aliyetaka kujua serikali inachukua hatua gani kuhakikisha wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu zaidi ya Elfu Nane kukosa mikopo kutokana na serikali kukumbwa na changamoto ya kuwa na mahitaji makubwa zaidi kuliko fedha inazokusanya.

Mh, Mizengo Pinda amesema kuwa serikali pia imeongeza idadi ya wanafunzi watakaopata mikopo hivyo wanasubiri hazina kutoa pesa hizo ili kumaliza deni hilo au kupunguza kwa kiasi Kikubwa.

Aidha Mh, Pinda ameongeza kuwa serikali haiwezi kusitisha, kutoa fedha kwa ajili ya kampeni za Kura ya Maoni ya katiba inayopendekezwa, au uchaguzi wa serikali za mitaa kwa ajili ya kuweza kulipia madeni ila itatafuta fedha za ziada kutatua matatizo yote yanayolikabili taifa.

Akijibu swali la mbunge Rajabu Mbaruk Mohamed aliyetaka nini tamko la serikali baada ya wafadhili kusitisha kuisaidia Tanzania, Mh. Pinda amesema wahisani wamekuwa na sababu tofauti ambapo kwa sasa wanadai wanangoja kuona taarifa ya mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali na iwapo wataikubali ndio wataweza kutoa hizo fedha jambo ambalo uamuzi huo unaenda kuathiri watu wengi badala ya watu wachache.

Aidha ameongeza kuwa kuwepo kwa taarifa za kupokea taarifa kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali Mhe. Pinda amesema Ofisi yake haijapokea taarifa hiyo na kuahidi kuifikisha taarifa hiyo bungeni punde kwa spika kama utaratibu unavyotaka.