Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,Mhe. George Simbachawene amesema serikali inatarajia kujenga vituo vipya vya afya takribani 105 kwa fedha ambazo zimetengwa kwa bajeti ya mwaka 2016/2017 ili kupunguza mahitaji yaliyopo kwa sasa nchini.
Waziri Simbachawene ameyasema hayo wakati akizungumza na East Africa Radio na kuongeza kuwa mbali na fedha za serikali katika ujenzi huo, wananchi nao pia watahusishwa katika michango mbalimbali ambayo itasaidia kukamilika kwa vituo hivyo kwa kuwa wananachi ndio wanajua mahitaji ya huduma za afya zinazohitajika kwa maeneo husika.
Amesema katika awamu hii ya nne wameamua kupeleka madaraka kwa halmashauri na wananchi wenyewe ili kupunguza malalamiko ambayo yamekua yakijitokeza mara baada ya miradi mingi ya serikali kujengwa bila kuzingatia mahitaji ya wananchi wa maeneo mbalimbali.
Amesema idadi hiyo ya vituo bado haitamaliza tatizo hilo kwa kuwa bado idadi ya watu inazidi kuongezeka hivyo watatumia mpango maalumu wakujumuisha Kata katika ujenzi wa vituo hivyo ili kuwafikia watanzania wote katika upatikanaji wa huduma za afya nchini.





