Saturday , 3rd Dec , 2016

Kijana David Mathew ambaye alipata ulemavu baada ya kupata ajali ya gari mwaka 2007, amesema watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto kubwa ya miundombinu rafiki ili kuweza kufanya shuguli zao mbali mbali za uzalishaji mali.

Akizungumza na East Africa Radio David amesema yeye akiwa miongoni mwa watu hao amekuwa mstari wa mbele katika kujishughulisha kuingiza kipato, lakini amekuwa akipata ugumu mkubwa wa mazingira kutokuwa rafiki kwake kwenye shughuli hizo.

"Kitu kikubwa ambacho kinatusumbua ni miundo mbinu, kwa mfano unasema nataka niende kufanya kitu fulani, unakutana na changamoto kama hizo za miundo mbinu unashindwa kufanya, sasa unaonekana kama huwezi kufanya kile kitu kwa sababu hakuna miundo mbinu ambayo inakusupport, lakini kama kungekuwa na miundombinu mbona unafanya kitu!", alisema David.

David aliendelea kusema kuwa changamoto hiyo imekuwa ni msumari wa moto kwao, hususan sehemu nyingi kukosa mazingira rafiki kwao, hivyo ameitaka serikali itoe amri maalum kwa kila ofisi za umma na binafsi kuweka mazingira rafiki kwa walemavu, ikishindwa basi ofisi hiyo inyimwe hadhi ya kuwa ofisi na kutoa huduma, kwani kuna watu wenye ulemavu wana uwezo mkubwa isipokuwa wanashindwa kutokana na changamoto hiyo.

"Taasisi nyingi za serikali hazina miundo mbinu za watu wenye ulemavu, umefika muda wa field naomba field, pale chini kwenye CV yangu nilikuwa nimeandika nina tatizo hili, ofisi nyingi zikawa zinawaza huyu mtu tunamuweka wapi, serikali kama inaweza iseme lazima kuwe na miundo mbinu inayoweza kuwafaa watu wenye ulemavu, vitu kama hivyo vipo, sasa sielewi wanatufikiriaje, serikali ihakikishe au hata hizo private organisation, wanaweka mazingira mazuri kwa watu wenye ulemavu", alisema kijana David.

David hivi sasa ni mhitimu wa chuo kikuu cha Dar es salaam, na anatarajia kuingia kwenye soko la kutafuta ajira, lakini amesema anahofu na hali yake, ofisi nyingi zitashindwa kumchukua licha ya juhudi na uwezo alionao.

 

Kijana David Mathew akiwa kwenye studio za East Africa Radio.