Chama cha Mawakala wa Forodha nchini Tanzania TAFFA, kimeitaka serikali kupitia wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kuingilia kati suala la makampuni 210 ya forodha yaliyozuiwa kufanya kazi katika bandari zote nchini kwa madai kuwa hatua hiyo iliyochukuliwa na mamlaka ya bandari TPA itakuwa na athari kubwa kwa uchumi wa nchi.............
Rais wa TAFFA Bw. Steven Ngatunga, amesema hayo jijini Dar es Salaam leo, katika mkutano uliowakutanisha wafanyakazi na wamiliki wa kampuni zote za uwakala wa forodha, ambapo katika maelezo yake rais huyo wa TAFFA amesema hatua hiyo itaathiri pia maisha ya takribani watu elfu kumi ambao wameajiriwa kama wafanyakazi kwenye mnyororo mzima wa kiuchumi wa sekta ya uingizaji na utoaji mizigo bandarini.
Kauli ya Bw. Ngatunga imekuja siku chache baada ya serikali kuahidi kuunda tume ya uchunguzi, itakayokuwa na jukumu la kuchunguza sakata zima la wahusika wa upoteaji wa shehena za mizigo na mapato katika bandari nchini, tume ambayo rais huyo wa TAFFA amesema itabaini nani mhusika mkuu katika sakata hilo.



