Thursday , 17th Sep , 2015

Wadau wa elimu wameitaka serikali ijayo kuboresha sekta ya elimu hususan kuweka mitaala na miundo mbinu thabiti, ili iweze kuwa na tija na kutoa fursa za kujitegemea kwa vijana wengi wanapohitimu masomo yao.

Rai hiyo imetolewa na Mkaguzi wa shule za msingi Bi. naomi Mwakalonge, alipokuwa akiongea kwenye kipindi cha Super Mix kinachorushwa na East Africa Radio.

Bi. Naomi amesema katika elimu ambayo inatolewa sasa kulikuwa na mtaala wa masomo ya stadi za kazi ambao unamjenga mtoto kuweza kupata elimu ya kujitegemea, lakini kumekuwa na udhaifu mkubwa kwani pamoja na kuwepo kwa mtaala huo, hakuna vitendea kazi vitakavyowezesha wanafunzi kusoma kwa vitendo.

Mbali na hayo Bi. Naomi pia amesema miundo mbinu katika sekta ya elimu bado ni tatizo kubwa nchini, hivyo kuitaka serikali ijayo kuliangalia swala hilo kwa kina, ili kuwe na uwezekano wa kutoa elimu yenye tija itakayoweza kutatua changamoto za ajira.

Pia Bi. Naomi ametaka kuongezwa kwa vyuo vya ufundi akitolea mfano chuo cha veta, ili kuweza kuwasaidia watoto watakaohitimu elimu ya msingi kujiunga na elimu ya ufundi, itakayowajenga kitaaluma na kuweza kujiajiri.

"Kwanza wawezeshe walimu na mazingira ya shule kuwa na vifaa kwa ajili ya kupata huo ujuzi kwa ajili ya kujitegemea, lakini nje ya veta viongezwe vyuo vingine vingi vingi ili mtoto atakapomaliza darasa la saba aweze kuingia kwenye hivyo hivyo vingine kupata ujuzi angalau kwa miaka mitatu minne akihitimu aweze kujitegemea", alisema Bi. Naomi.

Nao wadau mbali mbali wakitoa maoni yao kwa njia ya simu kwenye kipindi hicho, wameitaka serikali ijayo kuboresha maslahi ya walimu pamoja na mazingira yao ya kazi, ili kuweza kuifanya kazi hiyo kwa moyo, pamoja na kuboresha mazingira na miundo mbinu ya shule za umma.