Thursday , 12th May , 2016

Watu saba wa familia moja katika kitongoji cha Nyigumba kijiji cha Sima wilaya ya Sengerema mkoa wa Mwanza, wameuawa kwa kukatwakatwa mapanga usiku wa kuamkia juzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Ahmed Msangi.

Tukio hilo lililoacha simanzi katika kitongoji hicho, lilihusisha ndugu watano wa tumbo moja wakiwamo wanafunzi watatu, walivamiwa usiku wa manane na watu wasiojulikana na kuanza kucharangwa mapanga kwa kukatwa-katwa kabla ya kuwamaliza.

Hata hivyo, mauaji hayo yameibua utata mkubwa kwa tukio na mazingira hayo yaliyoibua utata na simanzi kubwa lakini chanzo chake bado hakijafahamika.

Wakizungumza eneo la tukio kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanafamilia walidai usiku wa saa 8 usiku kuamkia jana, watu wawili waliokuwa na mapanga walienda katika nyumba ya wanafamilia hao na kuanza kuwashambulia huku wakianza marehemu Donald ambaye alipambana na wauaji hao lakini alizidiwa nguvu kabla ya kuangushwa chini na kumaliza.

Hata hivyo, ilidaiwa mama wa familia ambaye naye aliuawa katika tukio hilo, alijaribu kufungua mlango wa chumba walicholala wajukuu na watoto wake, lakini sababu aliyowapa mwanya wauaji kuingia ndani ya nyumba na kuanza kuwashambulia kwa mapanga.

“Wauaji hao walipojiridhisha kutimiza mauaji hayo, waliondoka na kutokomea kusikojulikana huku wakiwa wamevaa makoti meusi ili wasiwe kufahamika,” alisema mmoja wa mashuhuda hao.

Akithibitisha kutokea mauaji hayo katika eneo la tukio, Afisa Mtendaji wa Kata ya Sima, Tamali Lukonge na diwani wa kata hiyo, Lugata Makoye, aliwataja waliouawa ni mama mwenye nyumba, Augenia Kiwitega (64), Maria Philipo na Leonard Thomas, ambaye anasoma kidato cha nne Shule ya Sekondari Sima.

Wengine waliouwa ni Leornad Aloys (darasa la saba) na Mkiwa Philipo mwanafunzi wa darsa la tano wote wa Shule ya Msingi Ijinga, na wengine walifahamika kwa jina moja moja, Samson na Donald kutoka wilayani Ngara mkoa wa Kagera waliokuwa wakulima wa familia hiyo.

Lukonge alisema marehemu Kiwitega alikuwa mwalimu mstaafu na mjane wa marehemu Joshua Mbata.

Akizungumza na viongozi wa kitongoji hicho, mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Mwanza, Augustine Senga, aliahidi kupatikana kwa wauaji hao na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Katika tukio hilo, watoto wawili (majina yamehifadhiwa) wa familia hiyo walinusurika kuuawa baada ya kujificha chini ya uvungu wa kitanda.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema kitendo hicho kilichofanywa hakiwezi kuvumiliwa, hivyo kuliagiza jeshi la polisi kuhakikisha linawapata waliofanya mauaji hayo.

Akizungumza eneo la tukio, Mongella alisema wauaji hao watakapokamatwa, watafikishwa katika vombo vya sheria na kuchukulia hatua stahiki.