
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli amefuta sherehe za Uhuru za mwaka huu ambazo hufanyika Desemba 9 ya kila mwaka na badala yake siku hiyo itumike katika kufanya usafi katika mikoa yote nchini ili kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.
Agizo hilo la hilo la Rais wa Tanzania limetolewa leo na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue wakati alipofanya ziara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kuangalia utekelezaji wa maagizo ya rais Magufuli aliyoyatoa baada ya kufanya ziara katika Hospitali hiyo.
Balozi Sefue amewataka wakuu wote wa Mikoa, wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuandaa vifaa vya kuzolea taka na kuwataka watanzania wote kujenga tabia ya usafi kwani usafi unaanza na mtu binafsi.
Wakati huo huo Balozi Sefue ametoa siku tatu kwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuhakikisha kuwa mashine za MRI na CT Scan zinaanza kazi mara moja.