Friday , 4th Dec , 2015

Rais wa Tanzania,Dkt.John Pombe Magufuli ametoa siku 7 kwa wafanyabiashara waliokuwa wanakwepa kulipa kodi kuhakikisha wamelipa malimbikizo yao ndani ya siku hizo badala ya kuendelea kuficha makontena vinginevyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli akiongea Dk Reginand Mengi Mwenyekiti wa Umoja wa Sekta Binafsi nchini

Akizungumza katika mkutano kati yake na wafanyabiashara nchini Dkt.Magufuli amewataka wafanyabiashara kuweka maslahi ya taifa mbele katika shughuli mbalimbali za maendeleo na kuiwezesha nchi kuondokana na umasikini...

Dkt. Magufuli amesema katika siku hizo saba endapo maagizo yake hayatatekelezwa basi sheria itafuata mkondo wake huku akiwataka wafanyabiashara kuwa wazalendo na taifa katika kulea maendeleo.

Kwa upande mwingine ametoa angalizo kwa watendaji wa serikali wenye tabia ya kuchelewesha maamuzi katika suala la uwekezaji bila sababu za msingi kuacha vitendo hivyo ili kutoa fursa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika mkutano huo mwenyekiti wa Sekta binafsi nchini Tanzania Dkt. Reginald Mengi ameitaka serikali kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji pamoja na kushughulikia rushwa ambayo inaonekana kushamiri na kufifisha ndoto ya Tanzania kuwa taifa lenye kipato cha kati kutoka cha chini.