Wednesday , 11th Nov , 2015

Mbunge mteule wa Kigoma Mjini kupitia chama cha ACT WAZALENDO Zitto Kabwe, amemtaka Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kutumia mamlaka yake aliyonayo kuunda serikali ya mpito Zanzibar, ili kushughulikia tatizo la kisiasa linaloikabili.

Zitto Kabwe ameyasema hayo leo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kwenye ofisi za chama hicho zilizopo Kijitonyama jijini Dar es salaam, na kusema kuwa tatizo la Zanzibar sio la kikatiba bali ni la kisiasa lililoletwa baada ya kufuta matokeo ya uchaguzi, hivyo anashangzwa kwa Rais kuwa kimya mpaka sasa.

“Wiki inakatika tangu Rais aapishwe, hatujawahi kusikia akizungumzia mambo ya Zanzibar, inabidi aingilie kati tatizo la Zanzibar si la kikatiba ni la kisiasa, ni lazima limalizwe kisiasa, watu waliamua kufuta matokeo, sio vizuri kuona Rais anaishia tu kwenda Muhimbili huku wenzetu Zanzibar bado hawajapata viongozi kikatiba, Rais atumie mamlaka yake waunde serikali ya mpito, waangalie upya katiba ya Zanzibar ili mshindi atangazwe ”, alisema Zitto Kabwe.

Pamoja na hayo Zitto Kabwe amempongeza Rais Magufuli kwa kudhibiti safari za nje kwa viongozi na kufanya ziara za kushtukiza kwenye wizara na sehemu nyingine na kumtaka kuweka mifumo endelevu kwani kwa kufanya hivyo pekee hakutapunguza mianya ya rushwa.

“Napongeza hatua ya Rais wetu hasa kudhibiti safari za viongozi kuhusu safari za nje, hilo ni jambo kubwa, kwenda tu katika sehemu kushtukiza hilo halitapunguza tatizo la rushwa, tunaomba aweke mifumo endelevu”, alisema Zitto.

Pia Mh. Zitto amesema chama cha ACT WAZALENDO kipo tayari kufanya kazi na chama chochote, na endapo atapangiwa kufanya kazi kwenye moja ya kamati za Bunge atafanya iwapo ni kwa manufaa ya wananchi.

“ ACT itakuwa tayari kufanya kazi na chama chochote ambacho kitakuwa na ushirikiano kwa manufaa ya wananchi, Bunge lijalo nitafanya kazi kwenye kamati yoyote ile ambayo nitakuwa nimepangiwa na Spika”, alisema Zitto Kabwe.