Thursday , 14th Apr , 2016

Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Mhe. Raila Odinga ameikosoa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kwa kusitisha kesi dhidi ya uhalifu wa kibinadamu iliyokuwa ikiwakabili vigogo wa serikali ya taifa hilo.

Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Mhe. Raila Odinga.

Mahakama ya ICC ilifutilia mbali kesi dhidi ya Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto na mwanahabari Joshua arap Sang.

Rais Uhuru Kenyatta aliondolewa mashtaka dhidi yake Desemba mwaka 2014.

Watu zaidi ya 1,000 waliuawa na wengine maelfu kuachwa bila makazi vurugu zilipozuka nchini Kenya kufuatia mzozo kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Raila, ambaye alikuwa Waziri Mkuu baada ya ghasia hizo, anasema hatua hiyo ya ICC kuondoa mashtaka dhidi ya vigogo hao wa Kenya itajenga kasumba ya kiburi miongoni mwa viongozi wa Afrika.

Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Kenya alisema hatua ya mahakama ya ICC ya kufutilia mbali kesi za washukiwa wakuu katika ghasia mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini Kenya tangu taifa hilo lipate uhuru, itawafanya viongozi wengi barani Afrika kutozingatia mfumo wa sheria wanapotawala.

Amesisitiza kwamba kutokana na uamuzi huo wa ICC, viongozi wengi wa kiafrika watakuwa madikteta na hawataogopa kushtakiwa.
Raila Odinga ametoa kauli hiyo akiwa mjini Paris nchini Ufaransa.

Hata hivyo matamshi hayo yamepingwa vikali na baadhi ya wanasiasa nchini Kenya.

Chanzo BBC.