Friday , 23rd Jan , 2015

Watuhumiwa wawili wa Ujambazi wamekamatwa eneo la Darajani Zanzibar Baada ya kurushiana risasi na Polisi.

Mtuhumiwa mmoja wa ujambazi akipakizwa kwenye gari ya polisi

Jeshi la polisi Zanzibar kwa kushirikiana na wafanyabiashara wa machinga walioko darajani Zanzibar  wamefankiwa kuwakamata majambazi wawili  huku kukiwa na taarifa kuwa mmoja amefariki baada ya kutupiana risasi  na kusababisha  kizaazaa cha aina yake mjini Zanzibar.

Hali hiyo imetokea baada ya  polisi  kuanza  kuwasaka na kuwafuata majambazi hayo ambayo baada ya kuona wamenaswa  wakaamua kukimbia na kuingia maeneo ambayo yanatumiwa na wafanyabishara  wadogo wadogo maarufu kwa jina la  'dada njoo'

Baada ya kuingia katika maeneo hayo, ndipo wafanyabishara hao wakaanza kuwanasa nakuwabana majambazi hayo yaliyokuwa katika gari aina ya Noah yenye namba  za usajili ambazo inasemekana ni za bandia.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mjini Magharibi Muccadam Khamis amesema polisi bado inawasaka wengine ingawa amesema uchunguzi unaendelea  na kuthibitisha kuwepo kwa wananchi wanane ambao walipatwa mshtuko na wako hopitali ya Mnazi Mmoja  wakipata  huduma za matibabu.

Hata hivyo taarifa zilipatikana mjini Zanzibar zinadai kuwa jambazi moja ambaye anajulikana kwa jina la Khmais Mabunduki na ambaye alikuwa anasakwa na polisi kwa muda mrefu ndiye aliyefariki kutoakna na mapigano hayo, huku bado polisi wakiendelea kuwasaka wengine ambao wako katika mtandao mmoja.