Friday , 21st Sep , 2018

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Ndugu Humphrey Polepole, amesema utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi mkoani Mbeya unaosimamiwa na mkuu wa mkoa huo Albert Chalamila, ndio utakaomuondoa mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole (kushoto) na Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbeya.

Akiongea leo asubuhi kwenye kipindi cha East Africa Breakfast kupitia East Africa Radio, Polepole amesema, watu wanaelewa vibaya kauli za baadhi ya wakuu wa mikoa hususani wale wanaoongoza mikoa ambayo majimbo yake yanaongozwa na upinzani.

''Mkuu wa mkoa wa Mbeya anatekeleza Ilani ya CCM na hiyo ndio itakipa ushindi chama chetu na aliposema atamng'oa Sugu hakumaanisha kwa nguvu bali ni utekelezaji wa Ilani yetu ndio utamtoa na mkuu wa mkoa ndio msimamizi wa Ilani katika eneo hilo'', amesema.

Aidha Polepole amefafanua kuwa wakati viongozi wa upinzani wakilalamika kila siku, Chama cha Mapinduzi kwa kushirikiana na serikali, kinatatua changamoto za wananchi na mwisho wa siku watakwenda kuwaeleza kwenye uchaguzi na kuwaacha upinzani bila cha kueleza.

Kuhusu malalamiko mbalimbali kwenye chaguzi ndogo zilizopita ambapo vyama vya upinzani vililalamika kutotendewa haki ikiwemo kwenye kuchukua na kurejesha fomu za kugombea pamoja na kuondolewa kwa mawakala siku ya uchaguzi, Polepole amesema huko ni kutatufa huruma ya uongo.

''Tusipende kusema uongo kwa umma kutafuta huruma hiyo ni dhambi, upinzani kwasasa kila mtumishi wa umma awe mkurugenzi au mahakama wanaona ni mchawi wao hivyo hata pale wanapotakiwa kupata huduma wanakosa kwa sababu wameshajenga imani ya kwamba hawatapata haki'', amesema.

CCM imeshinda viti vya ubunge katika majimbo ya Ukonga na Monduli ambayo yalifanya uchaguzi mdogo Septemba 16, 2018, kufuatia waliokuwa wabunge wa majimbo hayo kupitia CHADEMA kujiuzulu na kujiunga na CCM, ambako pia walipata nafasi ya kugombea na kurudi kwenye nafasi zao. Wabunge hao wateule ni Mwita Waitara wa Ukonga na Julius Kalanga wa Monduli.