Wednesday , 26th Aug , 2015

Mgombea wa urais wa CCM Dkt. John Pombe Magufuli jana ameendelea na kampeni katika mikoa ya Katavi na Rukwa ambapo ameahidi kuondoa uhaba na upungufu wa madawa hosptalini ikiwemo kuwashuglikia watakaobainika kuiba dawa hizo.

Mgombea wa Urais kwa tiketi ya CCM Dk. John Pombe Magufuli akiwahutubia wananchi wa Sumbawaga mjini mkoani Rukwa,ndani ya Uwanja wa Nelson Mandela.

Akihutubia katika mkutano wa hadhara wilayani Nkasi Mkoani Rukwa Magufuli amesema endapo atachaguliwa wahudumu wanaoiba dawa katika hospitali nchini atawashughulikia kwa mujibu wa sheria ili kukomesha hali hiyo.

Dkt. Magufuli ameongeza kuwa tabia ya watu kwenda hospitali kutibiwa na kuambiwa wakanunue dawa kwenye maduka binafsi kwa kuwa vituo vya afya havina dawa hizo ataikomesha mara moja.

Aidha Waziri Magufuli amesema anafahamu bayana shida za wananchi wa mikoa hiyo zikiwemo za barabara za lami, umeme, maji, elimu, uhuru wa kufanya biashara na migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji na kwamba atatatua matatizo hayo iwapo wananchi watampa ridhaa ya kuingia ikulu mwezi Oktoba.