Friday , 5th Oct , 2018

Takribani wanafunzi 6433 wanatarajia kurudia mtihani wa taifa wa darasa la saba, Jumatatu na Jumanne ya, Septemba 8 na 9 mwaka huu, baada ya matokeo ya awali kufutwa kutokana na udanganyifu uliofanywa na walimu wa shule hizo.

Akizungumza na www.eatv.tv Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), Dkt Charles Msonde amesema gharama zote za uandaaji wa marudio ya mitihani hiyo zitagharamiwa na serikali kupitia mamlaka husika na sio mtu binafsi huku akishindwa kutaja kiasi halisi cha gharama za marudio ya mitihani hiyo.

“_Serikali ndiyo iliyotangaza wanafunzi kurudia mitihani na siku zote mitihani hugharamiwa na serikali kwani wao ndio wahusika wakuu, hakuna mtihani wowote wa taifa ambao umekuwa ukigharamiwa na mtu binafsi ”_, amesema Dkt Msonde.

Kwa upande wa serikali kupitia kwa Naibu katibu Mkuu, wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, Bi Maria Semakafu serikali imejipanga vizuri katika usimamizi wa mitihani na itahakikisha inaweka ulinzi wa kutosha katika maeneo yote ambayo mitihani itafanyika huku naye akikataa kutaja gharama halisi itakayotumika.

“_Mimi wizara yangu inasimamia sera na ubora wa elimu, ilo swali la gharama naomba ungelielekeza NECTA au TAMISEMI kwa kuwa ni kesi tayari ipo mahakamani, maana kosa lingine ni kwamba tayari wameshaisababishia hasara serikali na kuchezea akili za watoto kwahiyo hatuna data kamili kwa sasa,” amesema Semakafu._

Kati ya shule zilizokumbwa na mkasa huo wa kurudia mitihani ni pamoja na, Kisiwani, Alliance na New Alliance za jijini Mwanza. Zingine ni Hazina, New Hazina, Aniny Nndumi na Fountain of Joy za Dar es salaam pamoja na shule zote za halmashauri ya Chemba na shule ya kondoa Intergrity za mkoani Dodoma.

Mpaka sasa uchunguzi unaendelea kufanyika kwa mahojihano kati ya walimu wakuu wa baadhi ya shule na wasimamizi wa mitihani iliovujishwa, huku baadhi yao wakikiri kusambaza ujumbe wa taarifa za mitihani kupitia mtandao wa whatsapp uliopelekea kufutwa kwa matokeo hayo.