
Jaji Semistocles Kaijage
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage na kusema zoezi la kuchukua fomu za uteuzi litakuwa kati ya Septemba 7 hadi 13 mwaka huu, ambapo uteuzi wenyewe utafanyika Septemba 13, 2018 huku akitaja tarehe ya kampeni kuanza Septemba 14 hadi Oktoba 12.
"Tume inavikumbusha vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, maadili ya uchaguzi, miongozo, na maelekezo yote wakati wa kipindi cha uchaguzi huo mdogo", amesema Jaji Kaijage.
Uwepo wa uchaguzi huo wa marudio umekuja baada ya kujiuzulu kwa Mbunge jimbo la Liwale kwa tiketi ya chama cha Wananchi (CUF), Zuberi Mohamed Kuchauka, ambaye alijiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) kumfanya apoteze sifa ya kuwa Mbunge na kulifanya jimbo hilo kuwa wazi.
Katika kipindi cha hivi karibuni, kumekuwepo na wimbi kubwa la Wabunge kutoka vyama vya upinzani kung'atuka nafasi zao na kuhamia upande wa chama tawala (CCM), hasa hasa kutoka CUF kwa kile wanachokidai ni kuwepo kwa migogoro ndani ya chama hicho jambo ambalo linawafanya kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.