Friday , 8th Jul , 2016

Shirika la Maendeleo la Taifa NDC limeanza utengenezaji wa mashine na vipuli kwa ajili ya kuongeza thamani bidhaa na mazao ya kilimo, hatua inayochochea kasi ya utekelezaji wa mpango wa serikali wa ujenzi wa viwanda.

Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano kwa Umma wa NDC Bw. Abel Ngapemba

Shirika la Maendeleo la Taifa NDC limeanza utengenezaji wa mashine na vipuli kwa ajili ya kuongeza thamani bidhaa na mazao ya kilimo, hatua inayochochea kasi ya utekelezaji wa mpango wa serikali wa ujenzi wa viwanda na hivyo kuiwezesha Tanzania kuwa taifa la uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Akizungumza katika mahojiano na Hotmix jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano kwa Umma wa NDC Bw. Abel Ngapemba, ametaja baadhi ya mashine hizo kuwa ni zile za kukamua na kusindika mafuta na vyakula pamoja na vipuri kwa ajili ya mashine zinazotumika kwenye viwanda vyote vikubwa vilivyopo nchini.

Kwa mujibu wa Ngapemba, mashine na vipuri hivyo vinatengenezwa kupitia kiwanda chake cha Kilimanjaro Mashine Tools kilichopo mkoani Kilimanjaro, ambacho hivi karibuni serikali imeamua kukifufua kwa lengo la kusukuma mbele ajenda ya ujenzi wa viwanda.

Wakati huo huo, taasisi isiyo ya kiserikali inayoundwa na wanawake ya Mbalawala Women Group iliyopo mkoani Ruvuma, imebuni mradi wa biashara ya makaa ya mawe ambapo wakazi kutoka vijiji nane vya wilaya za Mbinga na Songea mjini, wameachana na matumizi ya kuni na ukataji misitu kama chanzo chao kikuu cha nishati kwa ajili ya kupikia katika makazi yao.

Taasisi hiyo ni moja ya shughuli za kimaendeleo zilizobuniwa na wananchi katika maeneo ambako Shirika la Maendeleo la Taifa NDC lina miradi yake ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha wananchi katika maeneo hayo wananufaika moja kwa moja na miradi inayoendeshwa shirika hilo la maendeleo la taifa.

Meneja Miradi wa Taasisi hiyo Bi. Hajiri Mathew Kapinga amesema biashara hiyo imeanzishwa kwa msaada wa mgodi wa makaa ya mawe wa Ngaka uliopo wilayani Mbinga kwa lengo mahususi la kuwainua kiuchumi wanawake wanaouzunguka mgodi huo sambamba na kuachana na uharibifu wa misitu.

Bi. Kapinga ameongeza kuwa hata ukataji miti kwa ajili ya mkaa umepungua kwa kasi baada ya wafanyabiashara wa mkaa nao kujumuishwa katika uuzaji wa makaa ya mawe na hivyo kuachana na ukataji miti.

“Mradi wa makaa ya mawe kwa ajili ya kupikia umesaidia sana harakati za utunzaji wa mazingira....tumefanikiwa kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya mkaa baada ya kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wa mkaa nao wanawezeshwa na kuwa sehemu ya wauzaji wa mkaa unaotokana na makaa ya mawe,” amesema Bi. Kapinga

Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa mgodi huo Bw. Edward Mkony amesema Tanzania imeanza kunufaika na uwepo wa makaa ya mawe ambayo hivi sasa yanatumiwa na viwanda vingi nchini huku ziada inayobakia ikiuzwa nchi za jirani ikiwemo Rwanda.