Tuesday , 1st Dec , 2015

WAFANYAKAZI 38 wa kiwanda Yuko’s Enterprises (E.A) kilichoko Kiluvya Plot no. 23, wilayani Kisarawe mkoani Pwani wamefukuzwa kazi baada kukataa kusaini mkataba wa kazi ambao ulikuwa na mkanga nyiko.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Uledi Mussa

Ilidaiwa kuwa mgogoro huo unaohusu mikataba kati ya wafanyakazi na mwajiri huyo aliyejulikana kwa jina la Magoma Masegesa Magela ni wa muda mrefu na kuwa wamekuwa kisainishwa mikataba kiholela bila kufuata sheria na taratibu za kazi ambapo hadi sasa wana mikataba mitatu ambayo inawachanganya.

Mbali ya mikataba hiyo wafanyakazi hao wamedai kuwa mkurugenzi huyo amekuwa akiwanyanyasa kwa kushindwa kuwatimizia madai yao na kuwacheleweshea mishahara na kuwa inadaiwa amekuwa akijivunia kuwa waziri mkuu Kassim Majaliwa ni ndugu yake hivyo hawezi kufanywa lolote, waende popote wakashtaki.

Mwenyekiti wa wafanyakazi hao Silvester Kilosa alifafanua kuwa awali mwajiri huyo aliwasainisha mkataba wa miaka miwili ambao ulikuwa mwaka 2013 Januari hadi Desemba 2014, ambapo ulipoisha aliwasainisha mkataba mwingine wa miaka minne ambao ulianza mwaka 2015 hadi 2018 , lakini kabla hawajajua hatma ya mkataba huo mkurugenzi huyo aliwataka wasaini mkataba mwingine wa miezi miwili ambapo ulitakiwa uanze tarehe moja Desemba 2015 na kuisha tarehe 31 Januari 2016, ambapo walionyesha wasiwasi kuwa huenda ni mbinu za mwajiri za kutaka kuwafukuza kazi kijanja.

Alisema hata hivyo mwajiri huyo hajawahi kuwapa nakala ya mikataba huo wa miaka minne licha ya kuwasainisha na kuwa wamekwisha kumwandikia barua na kusisitiza kutaka nakala hizo alikataa na badala yake alileta mkataba huo mpya wa mwaka mmoja na kuwataka wasaini tena.

Wafanyakazi hao baada ya kutolewa nje ya kiwanda hicho waliamua kuandamana hadi ofisi za Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) zilizoko mjini Kibaha kwa ajili ya kupeleka malalamiko yao.

Katibu msaidizi wa TUICO mkoani Pwani Bernad Mkwati alisema tayari wanashughulikia mgogoro huo na kuwataka wafanyakazi hao wawe watulivu katika kipindi cha kusubiri madai yao yakishughulikiwa.

Hata hivyo wafanyakazi hao wamesema hawajajua wataishije katika kipindi ambacho TUICO inaendelea kufuatilia madai yao kwani mwajiri huyo alisema hata mshahara wa mwezi novemba hawatapewa.

Waandishi wa habari walifika katika ofisi za kiwanda hicho kwa ajili ya kupata ufafanuzi juu ya madai ya wafanyakazi hao lakini hawakupewa nafasi ya kumuona mkurugenzi wa kiwanda hicho badala yake walikutana na meneja uajiri ambaye naye pia hakuweza kutoa ushirikiano.