Thursday , 13th Sep , 2018

Kauli ya Spika wa Bunge ya kuwapiga marufuku Wabunge wanawake wenye kucha na nywele bandia imepokewa kwa hisia tofauti, wapo wanaounga mkono hoja ya Spika na baadhi wameikosoa kuwa anaingilia uhuru wa watu.

Juzi Bungeni jijini Dodoma Spika Job Ndugai alipiga marufuku Wabunge wanawake kuingia Bungeni wakiwa wamebandika kope na kucha bandia.

Kwa mamlaka niliyopewa na Bunge, napiga marufuku kuanzia leo hakuna mbunge atakayeingia ndani ya Bunge akiwa amebandika kucha au kope za bandia na suala la kujipodoa bado natafuta ushauri na majadiliano na wenzangu.”

Www.eatv.tv imefanya mahojiano na baadhi ya Wabunge wanawake  ili kupata maoni yao ambapo wapo waliopingana na Spika huku wengine wakionesha kuunga mkono na wengine kukataa kuzungumzia amri hiyo akiwemo Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Catherine Magige,amebanwa na shughuli za  kampeni katika la  jimbo la Monduli hazungumzii masuala ya Bungeni kwa sasa.

Kwa upande wake Ester Bulaya Mbunge wa Bunda Mjini (CHADEMA),  amesema kauli ya Spika inapaswa kupingwa na Wabunge wanawake kwa sababu huo ni udhalilishaji. “Kila mmoja ana uhuru wake wa namna ya kujipamba, akifanya hivyo, atakuwa anaingilia uhuru wetu, kwa nini, Spika hakuzungumzia madhara ya uvutaji wa sigara kwa wabunge wanaume?”, amehoji Bulaya.

Zainab Vullu Mbunge Viti Maalumu (CCM) amesema kauli ya Spika liwe funzo kwa wanawake wote, si wabunge pekee kwani kila mwanamke akitambua madhara yatokanayo na vipodozi, atawajibika sasa kutunza asili ya ngozi na viungo vyake alivyozaliwa navyo badala ya kuvibandikia vya bandia.

Mbunge mwingine aliyepinga amri ya Spika ni Rhoda Kunchela Viti Maalum, (CHADEMA), ambaye amesema kabla ya kutoa amri hiyo, Naibu Waziri wa Afya alishasema kucha na kope hazina madhara, bali inategemea na matumizi yake hivyo hakukuwa na sababu ya kupiga marufuku.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Faustine Ndugulile akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Fatma Tawfik, lililohoji kuwa ni wanawake wangapi wamepata madhara ya macho kutokana na matumizi ya kope bandia ambapo amesema kuwa kucha za bandia na kope sio vipodozi kwa mujibu wa sheria ya chakula na dawa ya vipodozi na kutoa takwimu kuwa wagonjwa 700 hupokelewa na hospitali ya Taifa ya Muhimbili kila mwaka kutokana na kutumia vipodozi vyenye kemikali vikiwemo vidonge vya kubadili rangi zao za asili hivyo kupelekea ongezeko la saratani kutokana na matumizi ya vipodozi visivyotakiwa.