Wednesday , 10th Feb , 2016

Hospitali ya Taifa Muhimbili imekiri mabadiliko makubwa tangu alipoingia madarakani Rais Dkt. John Magufuli katika kuwahudumia wananchi wanaokwenda kupata huduma ya matibabu hospitalini hapo.

Hayo yamesemwa hii leo na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo Prof. Lawrence Museru alipokuwa akizungumza na wanahabari na kuongeza kuwa sasa hivi wagonjwa wanapata dawa kwa asilimia 96% kupitia maduka yaliyoanzishwa hospitalini hapo.

Pia hospitali hiyo imeweza kulipa malimbikizo ya muda mrefu ya wafanyakazi ambayo yalikuwa ya kiwanyima morali ya kufanya kazi na kufanya utendaji wao sasa kuwa na mafanikio makubwa.

Aidha Prof Museru ameongeza kuwa hospitali hiyo imeweza kuongeza ukusanyaji mapato kwa zaidi ya asilimia 60 ambapo kuanzia mwezi Disemba hospitali imekusanya kiasi cha bilioni 3.3 kutoka kiasi cha bilioni 2.7 kiasi ambacho kilikusanywa mwezi Julai 2015 hadi Novemba 2015.

Kwa upande wa mashine mpya ya CT Scan Prof Museru amesema tangu kununuliwa kwa mashine hiyo kumewezesha wagonjwa zaidi ya 1000 kufanyiwa vipimo, pia kutengenezwa kwa mashine ya MRI kumewezesha wagonjwa zaidi ya 2200 wamefanyiwa vipimo.