Mh. Mnyeti ameyasema hayo jana akizungumza katika mkutano wa hadhara kata ya Haydom wilayani Mbulu, ambapo amesema ni vyema madiwani wa CHADEMA wakajiunga na CCM kwani yupo tayari kupokea simu ya diwani wa CCM hata akipigiwa usiku wa manane, ili kumpa msaada lakini si diwani kutoka vyama vya upinzani.
Amesema diwani wa CHADEMA ni ngumu kufanikisha maendeleo ya wananchi kwa madai kuwa, hakuna ambaye atamsikiliza akiwasilisha hoja zake katika vikao vya halmashauri husika.
"Hata hapa Haydom najua ni ngome ya Chadema hata mwenyekiti wa kijiji namuona ana damu ya CCM, sasa ondokeni huko mje huku tutekeleze ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 hadi 2020 kwa kuleta maendeleo," amesema Mnyeti.
Pia, amewataka watumishi wa halmashauri hiyo kutekeleza na kufanikisha kwa vitendo ilani ya CCM hata kama hawana kadi ya chama hicho kwani ndicho ambacho kipo madarakani.
"Mtekeleze hayo kwa nia safi, hiyo ni sawa na imani kwani hata kanisani huwezi kusikia padri akimsifu Muhammad na pia kule msikitini imamu huwa hamsifu Yesu," amesema Mnyeti.
Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Mbulu, Nasaeli Sulle alimhakikishia Mnyeti kuwa wananchi wa Haydom wamejitambua kuwa walifanya makosa na kuchagua CHADEMA ila sasa wapo tayari kuwachagua viongozi wanaotokana na CCM

