Mnara wa Saa katika jiji la Arusha
Akizungumza leo na waandishi wa habari ofisini kwake, wakati akijitambulisha, amesema tangu ateuliwe na Rais John Magufuli na kuja Arusha, alitembelea maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha na kuangalia kila Idara za Halmashauri hiyo ili kujiridhisha na kazi wanazofanya kama zinaendana na utoaji huduma bora kwa wananchi kama agizo la Rais.
Amesema cha kusikitisha amegundua madudu mengi, likiwemo la baadhi ya wataalam wa ardhi kutoa hati moja ya kiwanja kwa watu watatu, jambo linalosababisha migogoro inayotishia hata kupoteza uhai wa wananchi.
Kihamia amesema hali hiyo hakubaliani nayo na wahusika waliofanya hivyo wote watasakwa kokote waliko hata kama wamehama, watatafutwa na kuwajibishwa kwa kadri inavyowezekana, ili iwe fundisho kwa watumishi wengine.
Pia amesema ameweza kugundua baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo, kuchelewa kufika kazini, ambapo watumishi 50 ndani ya siku 28 alizokaa ofisini wamechelewa kufika ofisini bila sababu za msingi na kati yao hao 18 idara ya fedha.
Amesema watumishi hao wametakiwa waandike barua kujieleza kwa nini wamechelewa kufika ofisini wakati yeye anawahi saa 1:00 hadi 1:15, huku wakifahamu muda wa kazi na majibu yao, akiona ubabaishaji mtasikia hatua atakazochukua dhidi yao.
Aidha ametaja madudu mengine aliyokutana nayo ni shule ya Sekondari Olasiti, ambapo alifanya ziara ya kushtukiza na kubaini wizi wa mchele kilo 50 stoo.
Amesema alipomuuliza mwalimu mkuu Paulina Bagoye, alijikanyaga hakuna majibu ya msingi na muhusika wa wizi huo ni Judica Japhet, ambaye ni mtu wa Stoo na sasa mzazi, lakini mchele umeibiwa huku kufuli halijavunjwa wala mlango.
Amesema amemwagiza mkaguzi wa ndani kutembelea ghafla shule hiyo na kuendelea kuikagua na akijiridhisha baada ya taarifa ya mkaguzi wa ndani atamsimamisha kazi Mwalimu mkuu huyo na mwenzake aliyehusika.
Alisema hivi sasa hataki uswahili, watumishi wafanye kazi na ili kuwadhibiti watumishi wake, ameanzisha dawati la malalamiko na lazima yapatiwe majibu ndani ya siku saba, huku yeye mwenyewe akijipangi kila wiki siku moja atasikiliza kero za wananchi na siku moja kwa mwezi kusikiliza kero za watumishi wadogo, lengo kila mmoja apate huduma bora.



