
Akizungumza na East Africa Radio afisa afya mkoa wa Njombe Mathias Gambishi amesema kuwa katika halmashauri zote mkoa wa Njombe, zinatimiza kampeni za usafi wa mazingira na uboreshaji wa vyoo na kufanya maonesho ya wiki ya usafi wa mazingira.
'Maadhimisho haya yanafanyika kitaifa na mkoa wetu umechaguliwa kuwa mwenyeji, lakini jukumu la kuhakikisha maadhimisho haya yanafanyika vizuri na ukamilifu ni jukumu la watu wote wa mkoa wa Njombe, ikiwa ni pamoja na Halmashauri, sekretarieti ya mkoa, NGOs mbalimbali lakini pia na wananchi kwa ujumla wakishirikiana na viongozi wao, lakini wasimamizi wakubwa wa maadhimisho haya ni wizara ya afya na ustawi wa jamii ambao ndio waratibu pia wa kampeni ya afya na usafi wa mazingira", alisema Gambishi.
Pamoja na maadhimisho hayo Bwana Gambishi ameelezea changamoto wanazokabiliana nazo mkoani humo katika kutekeleza suala la usafi wa mazingira na uchimbaji wa vyoo.
"Tulikuwa na vizingiti kadhaa hapa katikati wakati wa siku za uchaguzi, kuna wanasiasa wanadhani jukumu la kujenga choo ni jukumu la serikali, changamoto nyingine ni ukosefu wa usafiri kuwafikia wananchi na fedha inayotokana na serikali imekuwa haifiki kwa wakati, kwa hiyo tukiweza kuwafikia watu wote, lengo tulilowekewa na serikali tutalifikia kwa wakati pia", alisema Gambishi.
Gambishi pia amesema kuwa katika wiki hiyo kututakuwa na maonesho mbalimbali ya usafi wa mazingira, unawaji na utumiaji bora wa choo pamoja na uchimbaji wa vyoo.