Saturday , 9th Jul , 2016

Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli amekumbushwa kupitia upya mikataba ya kimataifa na kikanda inayotaka kuwepo na misingi ya usawa wa kijinsia kwenye ngazi mbalimbali za uongozi.

Wito huo mekuja mara baada ya Mashirika yanayotetea haki za wanawake na usawa wa kijinsia nchini kulalamikia uteuzi ambao rais Magufuli amekuwa akiufanya katika ngazi mbalimbali za kimaamuzi nchini, kuwa nafasi hizo haziwapi wanawake fursa kulingana na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania iliridhia.

Akiongea na waandishi wa habari hii leo jijini Dar es salaaam kwa niaba ya mashirika mengine, Mkurugenzi wa mtandao wa jinsia nchini TGNP Bi. Lilian Liundi Ametaja nafasi hizo kuwa uteuzi wa baraza la mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa idara na taasisi, wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na maofisa tawala na wakufugenzi wa almashauri nchini.

Katika nafasi hizo idadi ya wanawake imepungua sana kulinganisha na idadi ya wanawake waliokuwepo katika utawala wa awamu ya nne ambapo usawa wakijinsia kwa kiasi kikubwa ulizingatiwa na wanawake kuweza kuwa miongoni mwa watenda maamuzi katika ngazi mbalimbali za uongozi

Bi. Lilian Liundi ameeleza kuwa tangu uteuzi huo ufanyike kiwango cha idadi ya wanawake kwenye nafasi za maamuzi imepunguwa kwa kiasi kikubwa jambo mbalo ameeleza kuwa linarudisha nyuma juhudi za kuziba pengo lililopo kuelekea usawa wa 50/50.

"Washauri wa rais wamkumbushe juu ya usawa wa kijinsia, hii inaturudisha nyuma kwa kiwango kikubwa, kibaya zaidi hata mwanamke akiteuliwa nafasi ya kuonyesha jinsia haiwekwi na inakuwa vigumu kutambua nani ni mwanamke nani ni mwanaume, jambo hili ni muhimu sana kwa ustawi wa jamii ya wapenda maendeleo" amesema Lilian Liundi