Wednesday , 13th May , 2015

Serikali imeiagiza ofisi ya mganga mkuu wa mkoa wa Arusha, kuwapandisha vyeo wauguzi wenye sifa, wapandishwe mara moja na kulipwa stahiki zao.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda

Agizo hilo limetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda, kwenye maadhimisho ya siku ya wauguzi, yaliyofanyika kwenye viwanja vya hospital ya mkoa wa Arusha, ya Mount Meru.

Katika hotuba hiyo iliyosomwa na Kaimu mkuu wa mkoa, Jowika Kasunga,ambaye ni mkuu wa wilaya ya Monduli, Ntibenda, amesema tayari maelekezo ya wauguzi kupandishwa vyeo yalishatolewa kilichobakia ni utekelezaji tu.

Amesema wapo wauguzi wana miaka sita hadi saba bila ya kupandishwa vyeo hivyo ni aibu, maelekezo yameshatolewa hakuna kizuizi kwa wauguzi kupandishwa vyeo, hivyo vema mganga mkuu akaondoa kero hiyo.

Amesema kupanda cheo kwa mtumishi yeyote ni haki yake, ili mradi tu ana sifa na vigezo na hiyo ni sehemu ya motisha katika utumishi.

Amewataka wauguzi kutunza vifaa vilivyopo sanjari na kuboresha huduma, ili kuongeza mapato ili kuwezesha kununuliwa vifaa vingine vya utabibu.

Pia amewaagiza wauguzi kusoma zaidi kwa kujiunga na vyuo mbalimbali, ili wapate fursa nyingi za kazi zao na kuongeza ufanisi.

Awali mganga mkuu wa mkoa wa Arusha, Dk. Frida Mokiti, amesema mkoa huo umefanikiwa kupunguza vifo vya watoto wachanga na wajawazito wakati wa kujifungua.

Amesema wauguzi wameendelea kuwa na moyo wa upendo wa kuwahudumia wagonjwa bila kujali muda licha ya kukabiliwa na changamo mbalimbali zilizopo.