Thursday , 7th Aug , 2014

Ofisi ya taifa ya takwimu nchini Tanzania leo imetoa taarifa ya mfumuko wa bei kwa kipindi cha mwezi Julai mwaka huu huku kukiwa na ongezeko kidogo ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwezi Juni.

Ephraim Kwesigabo, mkurugenzi wa sensa na Takwimu za kijamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini Tanzania.

Mkurugenzi wa sensa na takwimu za kijamii wa ofisi ya taifa ya takwimu Ephraim Kwesigabo amesema katika kipindi hicho mfumuko wa bei umeongezeka kwa wastani wa asilimia 0.1 kutoka asilimia 6.4 hadi asilimia 6.5.

Aidha Kwesigabo amesema thamani ya shilingi ya Tanzania nayo imezidi kuporomoka ambapo shilingi mia moja kwa sasa inaweza kufanya manunuzi yenye thamani ya shilingi Sitini na Saba tu.

Wakati huo huo, serikali ya Tanzania imekamilisha ujenzi wa kituo cha kupokea na kutuma mawasiliano ya mtandao wa intaneti kijulikanacho kama Intaneti POP, hatua itakayopunguza gharama za mtandao na kuongeza kasi ya mawasiliano ya simu pamoja na intaneti.

Kituo hicho kilichojengwa jijini Dar es Salaam, kitaondoa usumbufu uliokuwepo hapo awali ambapo Tanzania ilikuwa inategemea mawasiliano ya mtandao wa intaneti kutoka Marekani na Uingereza, hatua iliyosababisha gharama za intaneti kuwa za juu.

Aidha, mbali ya ujenzi wa kituo hicho, idadi ya nchi zinazonunua na kuunganishwa na huduma ya intaneti kutoa Tanzania nayo imeongezeka kutokana na kukamilika kwa ujenzi wa mkongo wa mawasiliano ambao umejengwa hadi katika mipaka na nchi za Uganda, Rwanda, Malawi na Zambia.