Saturday , 16th Jul , 2016

Mabingwa wa Soka Tanzania Bara timu ya Yanga leo imelazimishwa sare na medeama Sc ya kutoka Ghana katika mchezo wa wa Kombe la Shirikisho barani Afrika uliopigwa katika dimba la Taifa Dar es salaam.

Mshambuliaji wa yanga Donald Ngoma (Kushoto) akiwania mpira na mchezaji wa Medeama (Kulia)

Mchezo huo uliokuwa mgumu na wenye ushindani mkubwa umeshuhudia timu hizo ambazo zote ziko katika nafasi za chini zikifungana bao 1-1.

Yanga ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao mapema kabisa kupia kwa mshambuliaji wake Donald Ngoma kunako dakika ya 2 ya mchezo akipokea pasi safi kutoka kwa Thaban Kamusoko.

Bao hilo limedumu hadi dakika ya 17 iliposhuhudiwa likisawazishwa kupitia kwa Benson Danso, ambaye alimalizia kros ya mshambuliaji mwenzake, baada ya kupigwa mpira wa kona na mabeki wa Yanga kupoteza umakini.

Mchezo huo uliokuwa na msisimko wa aina yake umeshuhudia kosa kosa kadhaa kwa pande zote mbili kutokana na umakini wa washambuliaji wa timu hizo, ambapo kwa upande wa Yanga wachezaji Simon Msuva, Donald Ngoma na Chirwa walipoteza nafasi zaidi ya moja za wazi, huku Medeama wakishindwa kujiandikishia ushindi katika dakika za majeruhi baada ya mshambuliaji wake kukosa bao la wazi akiwa amebaki yeye na kipa.

Yanga iliwaanzisha washambualiaji wane ambao ni Tambwe, Ngoma, Msuva na Chirwa huku Kamusoko akiwa nyuma yao na Mbuyu Twite akicheza kiungo cha kukaba kwa lengo la kupata mabao mapema, lakini mpango huo haukufanikiwa hadi yalipofanyika mabadiliko ya kuwatoa Amis Tambwe na Oscar na nafasi zao kuchukuliwa na Juma Mahadhi na Haruna Niyonzima zikiwa zimebaki dakika takriban 20, mabadiliko ambayo hayakuzaa matunda zaidi ya kosakosa.

Kwa matokeo haya, Yanga imeendelea kubaki mkiani mwa msimamo wa kundi A kwa kujipatia pointi 1 ikiwa imepoteza michezo miwili, ikiwa nyuma ya Medeama yenye point 2 baada ya kupoteza mchezo mmoja na kupata sare mbili.
Mchezo mwingine wa kundi hili unapigwa kesho nchini Algeria kati ya MO Bejaia dhidi ya TP Mazembe.