Sunday , 17th Aug , 2014

Mwenyekiti wa chama cha NCCR Mageuzi ambaye ni Mwenyekiti mwenza wa kundi la Umoja wa Wananchi UKAWA, ameshangazwa na kile alichokiita kuwa ni upindishaji wa sheria juu ya uhalali wa kusitishwa au kutositishwa kwa Bunge Maalum la Katiba.

Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia.

Akizungumza wakati akitoa maazimio ya mkutano wa halmashauri Kuu ya chama hicho iliyokutana jijini Dar es Salaam; Mbatia ameonesha kushangazwa na kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema kuwa hakuna mwenye uwezo wa kusitisha bunge hilo.

Katika maelezo yake, Mbatia amehoji ni wapi bunge hilo lilipata uhalali wa kisheria wa kusitisha vikao vyake na kupisha vikao vya bunge la bajeti, huku ishara zikionesha kuwa bado bunge hilo litahitaji muda zaidi ya ule uliomo kwenye sheria wa kuendelea na mchakato wa katiba mpya.

Katika hatua nyingine, Mbatia ameshangazwa na kile alichokiita kuwa ni kukosekana kwa daftari la kudumu la wapiga kura huku Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikishindwa kufanya maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao licha ya muda kuwa umekwisha.

Kwa mujibu wa Mbatia, kukosekana kwa daftari linaloeleweka la wapiga kura sambamba na kutokwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi ni ishara mbaya kwa ustawi wa amani na demokrasia nchini.

Mbatia ameonya kuwa Tanzania inakabiliwa na tishio la kuingia katika machafuko ya wenyewe kwa wenyewe iwapo mapungufu hayo hayatashughulikiwa haraka iwezekanavyo.