Monday , 15th Jan , 2018

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma inakabiliwa na uhaba mkubwa wa damu salama ambapo kati ya chupa 1,000 hadi 1,500 zinazohitajika kwa mwezi zinazopatikana ni kati ya 700 hadi 800 tu na hivyo kupelekea uhaba mkubwa wa damu salama kwa wagonjwa.

Changamoto hiyo imetolewa na Mkuu wa kitengo cha Damu salama katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma Dk, Leah Kitundya wakati akizungumza na vijana wa Chuo kikuu cha Dodoma waliofika hospitalini hapo kwa ajili ya kuchangia damu kwa hiari.

Dk, Leah amesema kuwa tangu Mkoa wa Dodoma utangazwe kuwa makao makuu ya nchi kumekuwa na ongezeko kubwa la watu na ajali hivyo kupelekea uhitaji mkubwa wa damu salama ili kuokoa maisha ya wagonjwa.

"Ili tuseme kuwa tumekusanya damu ya kutosha tunatakiwa tupate damu 1000- 1500 kwa mwezi mmoja. Kwa jitihada zetu tumeweza kukusanya chupa chache kwa jitihada zetu. Hebu angalia 'gap' lililopo, naomba tuwe na utaratibu wa kuchangia damu. Watu wanapoteza maisha leo wao kesho utakuwa wewe", amesema Bi Leah