Monday , 29th Sep , 2014

Kamati ya Uandishi ya Bunge maalumu la Katiba imefanya majumuisho ya mwisho ya kuwasilisha rasimu ya Katiba inayopendekezwa ambapo alasiri hii imeanza kupigiwa kura.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba Mhe. Andrew Chenge.

Majumuisho hayo yamefanyika huku kifungu cha Rais wa Zanzibar kuwa makamu wa rais kikitolewa maelezo ya kina katika kuondolewa kwake kenye rasimu hiyo.

Akifanya majumuisho hayo Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi Mhe. Andrew Chenge amesema Kifungu hicho kimeondolewa kwa maslahi ya taifa kwa kuepuka migongano ya kisiasa endapo rais wa Zanzibar atatoka chama tofauti na rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania.

Wajumbe hao wanatarajia kupiga kura ya rasimu inayopendekezwa kuanzia alasiri leo hii mpaka siku ya Alhamis ambapo rasmu hiyo inatakiwa kupitishwa kwa theluthi mbili kutoka kila upande kabla ya kuipeleka kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya maoni.

Kura hizo zinapigwa huku vyama vya upinzani vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi UKAWA wakipinga kama ambavyo wamekuwa wakipinga vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, kwa madai kuwa mwenyekiti wa bunge hilo ameonyesha ukaidi kwa kuendelea na vikao hivyo na hata madai ya kutumiwa taratibu zitakazohalalisha kuwa kura hizo zimekidhi matakwa ya kisheria na kikanuni.