Miaka ya nyuma Afrika ilikumbwa na balaa ya njaa na kusababisha vifo vya watu, sio maelfu tu bali ni mamilioni.
Hapa tunakuletea majanga 10 makubwa yaliyowahi kutokea na kuua watu wengi zaidi, na nchi zilizoathirika.
1. Somalia (2010- 2011)
Ingawa hii ilikuwa ni miaka ya karibuni tu, lakini nchi ya Somalia ilipoteza watu takriban 260,000, kwa kipindi kifupi kutokana na njaa kali iliyoikumba, huku wengi wao wakiwa ni watoto chini ya miaka mitano ambao walikuwa takriban asilimia 10 ya idadi ya watu wa nchi hiyo.
Ingawa Umoja wa Mataifa ulishaona janga hili lakini ulikaa kimya na kusubiri mpaka pale ulipoua watu wengi zaidi, ndipo wakatangaza njaa kwenye nchi hiyo na kuitafutia misaada ya kimataifa.
2. Sudan (1998)
Mwaka 1998 nchi ya Sudan ilipitia kipindi kigumu kwa kupoteza watu takriban 70,000 kutokana na njaa na vita ya wenyewe kwa wenyewe.
.jpg)
Mama akimzika mwanaye aliyefariki kwa njaa nchini Sudan
3. Somalia (1991-1992)
Mwaka 1991-92, nchi ya Somalia ilikumbwa na tukio la njaa lililosababisha vifo vya watu zaidi ya 300,000, kutokana na kutokuwa na amani nchini mwao kulikotokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe, wakati wa utawala wa Mohammed Siad Barre, na kusababisha Umoja wa Mataifa kuingilia kati, na kutoa misaada ya chakula.

4. Ethiopia (1983 – 1985)
Hili limetajwa kuwa janga kubwa la njaa kuwahi kuikumba bara la Afrika, ambalo liliua watu takriban milioni moja nchini Ethiopia, na kutikisa dunia nzima. Karibia kila nchi yenye uwezo wa kusaidia iliisaidia Ethiopia kwa kupeleka vyakula na madawa. Lakini ilikumbwa na changamoto kubwa ya kiutawala na kuweka ugumu wa kuwafikia waathirika, na pesa zilizokuwa zikikusanywa na mataifa mbali mbali kusaidia, zilitumika tofauti kwa kununua silaha na vitu vingine ambavyo havikuwa hitaji kwa wakati huo, vyakula viliachwa vioze na kuongeza vifo zaidi.
5. Uganda (1980-83)
Wakati Ethiopia ikipoteza watu wake kwa njaa, nchi jirani ya Uganda nayo ilikuwa ikipitia hali hiyo hiyo, mwaka huo Uganda ilipoteza watu zaidi ya 30, 000.
6. Ethiopia (1950 – 1973)
Hii ilichukua muda mrefu zaidi, zaidi ya miaka 20, Ethiopia ilikuwa ikipoteza watu taratibu kutokana na njaa, lakini mwaka 73 hali ilikuwa mbaya zaidi na kuua watu zaidi ya 60,000. Mifugo ilikufa, mazao yalikauka, serikali ilikuwa ikikataa kuwa nchi imekumbwa na njaa, na kukataa misaada ya mataifa mengine.
7. Njaa katika ukanda wa Sahel
Sahel ni eneo lililopo Kaskazini mwa bara la Afrika, ambalo limepita kwenye nchi mbali mbali hasa zilizopo karibu na jangwa la sahara. Tangu miaka ya 1968 -73, ilikuwa ikikumbwa na njaa kali iliyotokana na ukame wa maeneo hayo yenye asili ya jangwa, na kuua mamilioni ya watu. Umoja wa Mataifa ulikuja na mkakati maalum wa kumaliza tatizo la uhaba wa chakula maeneo hayo, kwa kuanzisha program mbali mbali za kilimo.
8. Nigeria
Miaka ya 1967 – 1970, eneo moja lilipo nchini Nigeria liliamua kujitenga na kuanzisha nchi yake yenyewe, na kujiita Biafra, tukio hilo liliibua vita kubwa ya wenyewe kwa wenyewe na Nigeria, Kutokana na hilo serikali ya Nigeria ikafunga mipaka yake na kushindwa kupata huduma zote, hivyo ikasababisha njaa kali kutokea na kuua watu zaidi ya milioni 2. Nchi hiyo haikuweza kuendelea kwa muda mrefu, na hatimaye Nigeria ikachukua tena utawala wa eneo hilo. Kutokana na hilo, Nigeria ikatuhumiwa kuhusika kwa kusababisha njaa katika eneo la Biafra na kusababisha vifo vya mamilioni ya watu.

9. Ethiopia katika eneo la Tigray
Hii ilitokea mwaka 1958 katika eneo la Tigray nchini Ethiopia, na kuua watu zaidi ya 100,000.
10. Rwanda & Burundi
Mwaka 1945- 44, nchi za Rwanda na Burundi zilikumbwa na njaa, na kusababisha watu 36, 000 – 50,000 kufariki au kuikimbia nchi yao. Tukio ambalo lilisababisha wakimbizi wengi kwenye nchi jirani ikiwemo Kongo na Tanzania.





.jpg?itok=5cvL0YaP)