Tuesday , 14th Jun , 2016

Kata ya Saranga, Wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam sasa italazimika kurudi kwenye uchaguzi wa udiwani, baada ya  kubaki wazi kufuataia uamuzi wa Mahakama ya  Hakimu Mkazi Kisutu kutengua matokeo yaliyompa ushindi diwani aliyetangazwa.

Ephrahim Kinyafu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ndiye aliyetangazwa kuwa mshindi wa kiti hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 baada ya kuwazidi wagombea wengine akiwemo mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Yusufu Mdoe, ambaye Kinyafu alimzidi kwa kura zaidi ya 500.

Hata hivyo ushindi huo wa Kinyafu umetenguliwa leo na Mahakama ya Kisutu kufuatia kesi ya uchaguzi iliyofunguliwa mahakamani hapo na mgombea wa CCM bwana Yusufu Mdoe ya kupinga matokeo hayo.

Mahakama katika hukumu iliyosomwa na Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri kwa niaba ya Hakimu Mkazi Warialwande Lema, aliyesikiliza kesi hiyo na kuandika hukumu, amekubaliana na madai ya Mdoe na hivyo kutengua matokeo ya ushindi wa Kinyafu.

Katika hati yake ya madai na wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo Mdoe alikuwa akidai kuwa taratibu na kanuni za kuhesabu kura zilikiukwa, kwa kuwa kuna kura za moja ya vituo vya kupigia kura vya kata hiyo hazikuhesabiwa.

Upande wa utetezi (Kinyafu) ulipinga madai hayo ukidai kuwa hata kama kulikuwa na kasoro hiyo lakini haikuwa na athari katika matokeo ya jumla hata kama kura za kituo hicho zingeondolewa zisingebadilisha matoke kwa kuwa kura za kituo hicho zilikuwa 68 tu wakati tofauti ya kura kati ya mdai na mdaiwa ilikuwa ni kura zaidi ya 500.

Akizungumza na East Africa Radio baada ya hukumu hiyo, Wakili wa Kinyafu, Fredrick Kihwelu alisema kuwa hawajaridhika na hukumu hiyo na kwamba watakata rufaa katika Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo wa mahakama ya Kisutu jijini Dar es salaam.