Wednesday , 17th Aug , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Dawoodi Bohra Duniani Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin Saheb(TUS) Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli akifanya mazungumzo na viongozi wa Jumuiya Dawoodi Bohra

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Mufti wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir Ali na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Augustine Mahiga ambapo Rais Magufuli ameipongeza Jumuiya ya Dawoodi Bohra kwa juhudi kubwa inazofanya katika kutoa huduma za kiroho na pia kushiriki katika maendeleo.

Dkt. Magufuli amewakaribisha wana Jumuiya hiyo kuwekeza hapa nchini hususani katika sekta ya viwanda na pia amewakaribisha katika Maadhimisho ya Jumuiya ya Dawoodi Bohra duniani yanayotarajiwa kufanyika Jijini Dar es Salaam Mwezi Oktoba 2016.

"Tanzania ni nchi nzuri, tumekuwa na ushirikiano mzuri sana na wenzetu wa Jumuiya ya Bohra, hivyo njooni mfanye biashara na Tanzania, tumepanga katika kipindi cha mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021 Tanzania iwe nchi ya viwanda, kwa hiyo tunawakaribisha kuja kuanzisha viwanda vya kutosha" Amesema Rais Magufuli.

Kwa upande wake Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Dawoodi Bohra Mtukufu Dkt. Syedna Mufaddal Saifuddin Saheb amempongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri inayofanywa na Serikali yake ya awamu ya Tano, na pia ameahidi kuwa Jumuiya ya Dawoodi Bohra ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika maendeleo.