Thursday , 5th Nov , 2015

Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, ameapishwa rasmi leo na kukabidhiwa madaraka na rais anayemaliza muda wake Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Katika sherehe zilizofanyika kwenye viwanja vya Uhuru jijini Dar es salaam, Dkt. John Magufuli amekula kiapo cha kulitumikia taifa la Tanzania mbele ya Jaji mkuu Othman Chande, na viongozi mbalimbali wa kitaifa na wa dini.

"Mimi John Pombe Joseph Magufuli, naapa kwamba nitakuwa muaminifu kwa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, na nitalinda na kuitetea katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ilivyowekwa kwa mujibu wa sheria, ewe mwenyezi Mungu nisaidie", alisema Dkt. Magufuli alipokuwa akiapa.

Sambamba na Dkt Magufuli ambaye ndiye Rais wa awamu ya tano wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, makamu wa Rais naye Bi. Samiah Suluhu amekula kiapo hicho cha kuitumikia Tanzania kwa uadilifu na kwa bidii.

Mara baada ya kuapa mbele ya Jaji mkuu Mohamed Chande Othman, Dkt Magufuli amepigiwa mizinga 21 kama heshima kwake akiwa pia ndiye amiri jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama, na kisha kukagua gwaride kwa mara ya kwanza akiwa Rais.

Baadaye ndege za kivita zilipita mbele yake kama ishara ya heshima kwa amiri jeshi mkuu.

Mara baada ya gwaride maalum, zilifuata burudani mbalimbali na kisha Rais Magufuli kutoa neno la shukurani ambapo amewataka watanzania wote kuungana na kuacha tofauti zao za kisiasa ili kufanya kazi kwa maslahi ya taifa

Rais Magufuli alitoa shukrani zake kwa watu mbalimbali wakiwemo wagombea wenzake ambao walikuwa kwenye kinyang'anyiro hiko, na kuwataka kufanya kazi kwa pamoja ili kulijenga taifa.

"Nawashukuru wagombea wenzangu 7, nimejifunza mengi mema ambayo tumeyafanyia kazi, nyinyi mlikuwa washindani na si wapinzani, wote tuna kazi ya kuijenga Tanzania, nchi yetu daima ni kubwa kuliko vyama vyetu, uchaguzi umekwisha na sasa tushikamane tujenge taifa, hapa kazi tu na tuilinde amani ya Tanzania yetu", alisema Rais. Magufuli.

Miongoni mwa wageni waliohudhuria sherehe hizo kutoka nje ya nchi ni Rais Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Fellipe Nyussi wa Msumbiji, Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Robert Mugabe wa Zimbabwe, wawakilishi wa marais kutoka China, Ushelisheli, Umoja wa Ulaya, pamoja na mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania wakiongozwa balozi wa Uingereza Diana Melrose.

Baada ya tukio hilo katika uwanja wa Uhuru, Rais John Magufuli aliungana na wageni hao pamoja na marais wastaafu ikulu jijini Dar es salaam kwa ajili ya dhifa maalum.