Friday , 5th Aug , 2016

Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Tanzania kimepiga marufuku magari ya biashara na mabasi yasiyokidhi viwango ikiwa ni pamoja na daladala kukodishwa na mashule kwa ajili ya kuwasafirisha wanafunzi.

Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani Mohamed Mpinga akisisitiza jambo.

Jeshi la Polisi kikosi cha usalama barabarani nchini Tanzania kimepiga marufuku magari ya biashara na mabasi yasiyokidhi viwango ikiwa ni pamoja na daladala kukodishwa na mashule kwa ajili ya kuwasafirisha wanafunzi.

Akizungumza na East Africa Television mkuu wa kikosi hicho DCP Mohamed Mpinga amesema katika kuhakikisha wanazuia magari hayo yasiendelee kufanya shughuli hiyo wanayojiingizia kipato kwa njia isiyo halali, jeshi hilo limeweka mpango maalum wa kuyakamata mabasi hayo na kuyachukulia hatua stahiki za kisheria.

Kwa upande wa wazazi amesema wana jukumu la kuhakikisha wanafunzi wanakuwa salama kwa kukubaliana na wamiliki wa mashule waweke magari ambayo yanatambulika na SUMATRA ambayo ni lazima magari hayo yawe na rangi ya njano na yakidhi kiwango cha ubora kwa usalama barabarani.

Kwa upande wa bodaboda Kamanda Mpinga amesema tayari wamewakamata baadhi ya madereva wa bodaboda ambao wanawabeba watoto chini ya miaka 9 ikiwa ni kinyume cha sheria za usalama barabarani zinavyoelekeza.