Wednesday , 23rd Jul , 2014

Jeshi la polisi jijini Arusha limekamata mabomu saba, risasi na bunduki aina ya shortgun katika operesheni dhidi ya matukio ya mabomu jijini humo.

Mkuu wa jeshi la polisi nchini Tanzania IGP Ernest Mangu.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya Jinai DCI, Isaya Mngulu amesema kuwa mabomu hayo yamekamatwa Julai 21 mwaka huu, eneo la Sombetini, Manispaa ya Arusha, huku sita kati ya saba yamatengenezwa nchini Urusi wakati moja likiwa limetengenezwa nchni Marekani.

Aidha jeshi hilo limesema linawashikilia watu 25 kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya milipuko ya mabomu katika nyumba za ibada, mkutano wa CHADEMA, Mgahawa, na nyumba za viongozi wa dini.

Taarifa ya jeshi hilo imefafanua kuwa juzi Julai 21 majira ya saa 20.00 usiku maeneo ya Sombetini walikamatwa Yusuph Hussein Ally maarufu kama Huta, kabila Mrangi, umri wa miaka 30 na mkewe Sumaiya Juma, kabila mwasi, umri wa miaka 19 wakiwa nyumbani kwao na baada ya kupekuliwa walikutwa na mabomu ya kutupwa kwa mkono saba, risasi sita za shortgun, mapanga mawili, unga wa baruti unaokadiriwa kufika nusu kilo na bisibisi moja.

Mtuhumiwa Yusuph kwa mujibu wa polisi ni miongini mwa watuhumiwa waliokuwa wanatafutwa kwa ulipuaji wa mabomu maeneo yote jijini Arusha na kwamba polisi inaendeleo kumhoji kuhusiana na tukio hilo.

Polisi imeendelea kueleza kuwa uchunguzi wa shauri hili pamoja na matukio mengine ya milipuko unaendelea, ikiwa ni pamoja na kuwahoji watuhumiwa walioko mikononi mwa Polisi na kuwakamata watakao bainika kuhusika na matukio hayo.

Hata hivyo Jeshi la Polisi linatangaza kumtafuta Yahaya Hassan Hella, kabila mrangi, umri wa miaka 33, mkazi wa Mianzini Arusha, mwenye asili ya eneo la Chemchemu Kondoa mkoani Dodoma kwa tuhuma za kuhusika na matukio ya ulipuaji mabomu nchini na kwamba zawadi nono itatolewa kwa yeyote atakaye toa taarifa zitakazowezesha ukamatwaji wa mhalifu huyu.