
Kocha Marehemu James Siang'a
Katibu wa chama cha makocha wa mpira wa miguu nchini kenya (KeFOCA) Bob Oyugi amesema James Siang’a ambaye aliwahi kuichezea Gor Mahia, Luo Union, na timu ya taifa Harambee Stars kama goli kipa amefariki na kuacha pengo kubwa akiwa kama mtu mwenye mchango mkubwa katika soka la Kenya.
“Tumempoteza ndugu yetu siang’a ambaye alikuwa mtu mashuhuri kitaifa na kimataifa, amefariki usiku jana kulingana na maelezo ya ndugu wa familia yake. tunasubiri maelezo zaidi kuhusu taratibu za mazishi kutoka kwao na namna mambo yatakavyokuwa. roho yake ipumzike kwa amani” Amesema Oyugi.
Siang’a alikuwa mchezaji golikipa na baadaye akafika hadi ngazi ya kimataifa katika mechi mbalimbali nchini Kenya. alishiriki katika kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 1972 pia akawa meneja wa Kenya mwaka 1999 hadi 2000.
Alizidi kung’ara na kuingia nchini Tanzania ambapo alikuwa meneja wa Taifa Stars mwaka 2002, pia amewahi kuwa kocha wa timu mbalimbali katika ukanda wa Afrika mashariki kama Simba, Moro United na Express ya uganda . akiwa Moro United mwaka 2004 Siang’a aliombwa tena kuwa Kocha wa Taifa Stars kwa mara ya pili lakini alikataa.
Aidha simba itamkumbuka zaidi siang’a kwa kuwa kocha wa mwisho kutamba na simba kwenye ligi ya mabingwa afrika hadi sasa ambapo simba ilicheza na Zamaleck na kuifunga goli moja kwa bila mwaka 2003 na hakuna kocha aliyevunja rekodi hiyo.
Pia amewahi kuwa kocha wa mtibwa sugar baada ya hapo akaifundisha gor mahia ya Kenya na baada ya hapo alipewa heshima ya kuwa kwenye kamati ya washauri wa soka nchini kenya.
Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu amen.